Penzi laingia doa

Maafisa wa polisi mjini Molo wameanzisha msako mkali dhidi ya mwanamume mmoja aliyemuua mpenziwe katika mtaa wa Tayari wikendi hii.

Kwa mujibu wa majirani, wapenzi hao wamekuwa na mizozo ya kinyumbani na inakisiwa kuwa hii ndio sababu kuu ya mshukiwa, Moses Igunza wa umri wa makamu, kumwangamiza mpenziwe wa umri wa miaka 28, Anne Waithera kwa kumdunga kisu kifuani.

Kwa muda, wapenzi hao wawili walikosa kuonekana baada ya kuwa na ugomvi mkali uliovutia hisia za majirani, jambo lililowatia wasiwasi pia na kuamua kwenda kuangalia kilichojiri nyumbani kwao.

Katika boma lao, kulikuwa kumetulia tuli lakini majirani waliweza kuchungulia kupitia kwa mianya ya nyumba yao ya mbao na kuuona mwili wa Waithera ukining’inia kwenye sofa sebuleni.

Milango yote ilikuwa imefungwa na hivyo basi walipiga ripoti kwa maafisa wa polisi ili Waithera apate usaidizi.

Naibu mkuu wa polisi eneo hili Harrison Matheka alithibitisha kisa hiki akisema kuwa ni kisa cha unyama lakini hawatolegeza kamba hadi pale watakapompata Igunza na kumfungulia mashtaka kulingana na sheria.

Matheka alisema kuwa walikuwa wamepokea ripoti ya kupotea kwa Waithera kutoka kwa Wazee wa nyumba kumi na pindi tu walipoipata habari ya mtu kuwa ndani ya nyumba walifika mahala pale na kupata kuwa aliyekuwemo alikuwa Waithera na alikuwa ameshaaga.

Mahala pale pa tukio palipatikana na kisu kilichokuwa kimejaa damu kinachoaminika kutumika katika mauaji haya.

Aliwahimiza walio katika mahusiano ya mapenzi kutafuta ushauri mwafaka kutoka kwa wale watakao wasaidia iwapo wanakumbwa na changamoto ili kuepukana na matukio kama haya ya kinyama.

Mwili wa mwenda zake umepelekwa katika makafani ya hospitali ya gatuzi dogo la Molo ukingojea kufanyiwa upasuaji.

admin

admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *