Wakulima wadogo wadogo kutoka Magharibi mwa Kenya wamehimizwa kukumbatia mbegu mpya ya mtama aina Striga Smart Sorgum kama suluhu ya kumaliza kwekwe chawi (Striga ) shambani.
Striga Smart Sorgum ni teknolojia mpya iliyofumbuliwa na watafiti ili kupata suluhu kamili ya kuondoa kwekwe chawi kwa manufaa ya kukuza mtama kwa wingi miongoni mwa wakulima katika eneo la Magharibi mwa Kenya.
Mmoja wa watafiti wa kisayansi katika Chuo Kikuu cha Kenyatta Profesa Stephen Runo amesema kwekwe chawi imekua tishio kuu kwa wakulima na kupelekea usalama wa chakula nchini kudorora hivyo kutoa mwanya wa kuwepo teknolojia na mbinu mpya ya kukabiliana na kwekwe Chawi ipasavyo.
Profesa Runa amesema aina tofauti za mbegu mpya ya mtama yenye mazao mengi imefanyiwa utafiti na kupatikana kuwa na uwezo wa kupambana na kwekwe chawi hivyo kupelekea mkulima kupata mazao tele shambani.
Runo ameelezea kuwa utafiti wa majaribio tayari kumaliza kwekwe chawi umefanywa kwenye mashamba katika kaunti za Busia, Kisumu na Homa Bay ambazo zimekuwa kitovo cha kwekwe chawi kwa miaka mingi.
Akizungumza kwenye warsha ya Striga Smart Sorghum, iliyowaleta pamoja wanahabari, watafiti na wadau kutoka sekta mbalimbali, Profesa Runo anaamini kuzinduliwa kwa aina mpya ya mtama nchini itawaokoa wakulima kutokana na kiangazi ya muda mrefu inayosababisha njaa na uamasikini nchini.
Runo aidha amewahimizi wakulima kukumbatia ukulima wa mbegu mpya za mtama ambayo ina uwezo wa kuua kwekwe chawi pindi tu inapochipuka na kuenea shambani.
Hata hivyo,watafiti wameelezea kwamba mmea mmoja wa kwekwe chawi unauwezo wa kuzalisha zaidi ya mbegu 50,000 za vumbi zinazodumu kwenye ardhi kwa zaidi ya miaka 20.