Mwanachama wa jopokazi la kuthathmini mfumo wa masomo nchini Dkt. Jane Imbunya ameusifia mtaala mpya wa elimu unayojulikana kama CBC.
Dkt Imbunya, ambaye ni mtaalamu wa maswala ya mitaala na utafiti, amehoji kuwa CBC ni mtaala mwafaka ambao tayari umetekelezwa katika mataifa mengine kama vile Uchina na Brazil kwa ufanisi mkuu.
“Tetesi hapa nchini ni kwamba wananchi wa kawaida hawakuhusishwa, jambo ambalo kama jopo tunaenda kufanya,” alisema Dkt Imbunya, ambaye ni mhadhri katika chuo kikuu cha Marafiki cha Kaimosi.
Katika mahojiano ya kipekee na KNA, Dkt Imbunya anasema mtaala huu unatumia vigezo mbalimbali kutathmini wanafunzi kulingana na vipaji na uwezo wao bila ya kumlemea yeyote.
Matamshi yake yanajiri huku kukiwepo na tetesi kutoka kwa wazazi wakilalamikia gharama kubwa ya mfuma huu.
Wengi wa wazazi na wafadhili wa wanafunzi wanadai walimu wanaitisha vitu vingi vya kusaidia wakati wa vipindi vya utendaji.