Maafisa wa usalama katika kaunti ndogo ya Keiyo Kaskazini hii leo walishirikiana na vijana kupanda miti katika juhudi za kuimarisha uhusiano kati yao.
Hillary Kiplagat ambaye aliandaa shughuli hiyo ya upanzi wa miti alisema alitaka kuhusisha shughuli hiyo na udumishaji wa amani akisema wakati polisi na vijana wanapanda miti wanapata nafasi nzuri ya mazungumzo na hivyo basi kuweza kuelewana.
Akizungumza katika shule ya upili ya vijana ya St. Patricks Iten, Kiplagat alisema alichagua shule hiyo ya kitaifa kimaksudi akisema kwa vile wanafunzi wanatoka kila pembe ya nchi, basi wanapoenda nyumbani wataweza kueneza ujumbe wa amani.
Kiplagat alisema vijana wana jukumu kubwa la kulinda amani nchini kwani wanahitaji mazingira yaliyotulia ili kuweza kufanya kazi na kulinda kizazi cha kesho.
“Ni muhimu kama vijana tuhakikishe kuwa kuna amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu unaokuja kwani tunahitaji amani ili tujiendeleze kimaisha,” alisema Kiplagat.
Kwa mujibu wa mkuu wa polisi katika eneo hilo Tom Makori, vijana mara nyingi hutumiwa kuzua rabsha na kwa hivyo ushirikiano kati yao na polisi ni muhimu kwani wataweza kuripoti visa vyovyote bila kuwaogopa polisi.
Mkuu huyo wa polisi alisema ni muhimu kuhakikisha kuwa amani inadumishwa hasa wakati huu ambapo nchi hii inaelekea kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Akiongea baada ya upanzi huo wa miti, Makori alieleza kuhuzunishwa kwake na visa vya mauaji ambavyo vinaendelea kuripotiwa mjini Iten kutokana na ukatili wa kijinsia.
Makori alisema visa hivi havitokani na utovu wa usalama mjini Iten bali vita vya kinyumbani na kuwataka wakazi kutumia mbinu zote kusuluhisha matatizo kati ya wanandoa kabla ya kuwa tanzia.