Wafugaji waonywa dhidi ya kuharibu mashamba ya wenyeji Mwingi

Serikali imetoa onyo kwa wafugaji wa ngamia wanaoharibu mmea katika mashamba ya wakulima eneo la Kwa Kamari na Kasiluni, Tseikuru, Mwingi Kaskazini kwamba watafurushwa maeneo hayo.

Akizungumza alipozuru maeneo hayo ambapo kumeshuhudiwa mvutano baina ya wafugaji wa ngamia kutoka maeneo ya Garrisa, Tana River na Wajir na wakulima hao, Kamisheni Kaunti ya Kitui Erastus Mbui ametoa onyo kali dhidi ya kuchukua sheria mkononi mwao akisema serikali itafanya bidii kuhakikisha usalama na uhusiano mzuri umepatika katika jamii hizo mbili. Wakulima walielekezwa kuripoti kesi katika kituo cha polisi ili kuwezesha polisi kuchukua hatua za kisheria.

Akizungumza katika mkutano uliowaletea pamoja wafuga na wakulima pamoja, Mbui aliwaonya wafugaji kwamba yoyote atakayepatikana akilisha mifugo katika shamba la wenyewe atachukuliwa hatua za kisheria.

Jamii hiyo ya eneo la Kwa Kamari wamependekeza serikali kuibuni mipaka mpya ambayo itawezesha wao kuishi kwa amani na wenzao kutoka Kaunti za Tana River na Garissa wakihoji kwamba kwa miaka mingi mvutano kati yao na wafugaji ni tatizo la kutokuwepo na mipaka wazi kati ya kaunti hizo jirani.

Wenyeji hao pia wamehoji kwamba wafugaji wanawauzia mifugo na kurejea kudai mifugo hao baada ya wiki mbili wakidai walipotea na kuwa hawakuuza.

Wameiomba serikali ya Kaunti ya Kitui kuifungua rasmi soko la mifugo la Kamari kama njia moja ya kusuluhisha tatizo la wafugaji kudai mifugo baada ya kuuza.

Kamisheni Mbui alitoa agizo kwa wakuu wa usalama kaunti ndogo ya Tseikuru kujadiliana na wenyeji kutoka pande zote na kubuni kamati ya amani ambayo itakuwa ikisaidiana na serikali kuhakikisha uhusiano njema itakuwepo kati ya jamii ya wafugaji na wakulima.

Kamanda wa polisi kaunti ya Kitui Leah Kithei amewaomba wenyeji kuripoti kesi kwa polisi na pia kutoa ushahidi kama njia ya kusaidia polisi kuwakamata wavunja sheria.

Kwa miaka mengi kumekuwa na mvutano katika jamii ya wafugaji na wakulima katika eneo hilo na sasa wenyeji hao wana matumaini kwamba suluhu itapatika baada ya serikali kuweka mikakati kabambe kuona kwamba usalama unadumu maeneo hao. Wameiapa kushirikiana na serikali.

Wakuu wote wa usalama kauti ya Kitui pamoja na wachifu wa kaunti ndogo ya Tseikuru walikuwepo katika mkutano huo.

admin

admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *