Kipute cha daraja la pili kutifua kivumbi Wikendi

Baada ya kukamilika kwa ligi kuu daraja la kwanza nchini ambapo tulishuhudia wanangarambe wa Mayenje Santos na Kona Rangers wakipandishwa hadi ligi ya Super, kibarua sasa chaelekezwa kwa ligi kuu daraja la pili wikendi hii.

Mitanange hio itatinga raundi ya 23 wikendi hii huku vikosi mbalimbali vikijisatiti kupamba kurasa za mioyo ya mashabiki wao kwa mabao na mihemko ya soka ya kiufundi.

Mechi zote zimeratibiwa kung’oa nanga mida ya saa saba katika nyuga mbalimbali huku waamuzi mbalimbali walioongea na KNA wakielezea utayarifu wao wa kupuliza vipenga.

“Tupo radhi kuandaa mitanange hii pasi na mashaka kwa kuwa tunajisatiti kukamilisha ratiba za msimu huu mapema na kuanza maandalizi ya msimu ujao,” mwaamuzi wa kipute hicho Jacob Oburu alisema.

Jumamosi katika uga wa Sirens mjini Bungoma kutatifuliwa kivumbi huku Bungoma Altars FC wakiwaalika wageni wao Rosterman United FC mbele ya mashabiki wa nyumbani.

Kikosi cha Bungoma Altars FC kitajisatiti kutetea nafasi ya tatu katika jedwali hilo huku Sigalagala FC wakiwa tishio katika nafasi hio.

Katika shule ya msingi ya Mundika kule Busia, Green Canopy watawaalika Lugulu FC ambao wameboronga msimu huu kabla ya Sigalagala FC kuwavaa Butali FC katika uga wa nyumbani pale kwenye chuo anuwai cha Sigalagala.

Sigalagala wamekuwa na msimu imara huku wakiwa wameshikilia nafasi ya nne nyuma ya Altars ambao wamejitia kidedea kwa kutopoteza mechi zao tatu za hivi punde.

Marenga FC watakunja njamvi la michuano ya Jumamosi katika uga wao wa nyumbani watakapowaalika vinara wa kipute hicho Compel FC katika uga wa Lunyofu Grounds.

Compel wanapania kujitoa jino kwa ukucha kutetea taji ambalo limo mikononi mwao japo kwa asilimia ndogo huku Marenga wakitafuta ushindi ambao utakuwa ushindi mkubwa kwao msimu huu.

Jumapili kutaandaliwa mitanange matatu ya ndovu kumla mwanawe huku Lumakanda FC wakijitwika mikoba ya Shaviringa katika uchanjaa wa shule ya msingi ya Lumakanda. Lumakanda wanakaribia kucha za kushushwa daraja nao Shaviringa wakijititimua misuli kuingia tano bora wa msimu huu.

Washikilizi wa nafasi ya pili katika mapambano hayo Vihiga Sportiff FC watakuwa wageni wa Luanda FC ambao wana miadi ya kuingia tatu bora kwa mujibu wa mkufunzi wao.

Uchanjaa wa shule ya msingi ya Kipsis utatufungia ukurasa wa mitanange ya wikendi hii huku wenyeji Kipsis Arrows FC wakiwaandalia ubwabwa Youngstars FC.

Kwa mujibu wa Moses Akali mwenyekiti wa shirikisho la soka nchini FKF kanda ya Magharibi, mitanange hio imeratibiwa ipasavyo na kila mikakati ipo sadakta kuhakikisha kuwa kila kitu kinaenda kwa ushwari na upekee wa aina yake.

admin

admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *