Kipute cha Magharibi Kunoga Wikendi hii

Mashindano ya shirikisho la soka kanda ya Magharibi, daraja la pili yatanoga wikendi hii katika nyuga mbalimbali huku, vilabu husika vikijisatiti kuburudisha mashabiki wao.

Kipute hicho kitatinga raundi ya kumi na nane huku waburura mkia, Youngstars, Kanzu na Rush Legend wakijikakamua kukwepa shoka la FKF.

Mashindano hayo ambayo hutoa klabu moja kujiunga na ligi ya Super yanadhaminiwa na kamati shikilizi ya shirikisho la soka nchini FKF pamoja na wizara za michezo majimbo ya Bungoma, Busia na Kakamega mtawalia.

Jumla ya mitanange minane itatesa nyasi wikendi hii huku mitatu ikisakatwa mnamo jumamosi na hatimaye mitano kupigwa mnamo jumapili.

Mechi zote zitaanza mida ya saa saba mchana na wanasoka wote wameelezea matumaini yao ya kufanya vyema katika kipute hicho.

Kwa mujibu wa Bramwel Kibet mkufunzi wa timu ya Youngstars ambayo inashikilia nafasi ya 16 nyuma ya 11 Jaws, wanadinga wake wamejiandaa vilivyo kuwaandaa wapinzani wao na kunyakua alama zote tatu. Kibet aliyasema haya katika mahojiano ya moja kwa moja kwa njia ya simu na KNA.

Shaviringa United watakuwa wa kwanza kuwavaa Bungoma Allstars katika uga wa Kaimosi huku Allstars wakipania kunyakua alama zote tatu nao Shaviringa wakitafuta ushindi mbele ya mashabiki wa nyumbani.

Wakati huohuo katika uga wa shule ya msingi ya Muyayi viongozi wa ligi hio Compel FC wataalikwa na Youngstars ambao wanasaka kuimarisha matokeo yao baada ya msururu wa matokeo duni tangia mwanzoni mwa msimu.

Kule Cheptais Kipsis Arrows watawavaa 11 Jaws FC nyumbani na kufunga mitanange ya Jumamosi.

Siku ya Jumapili itakuwa siku ya kufa mtu huku mechi tano zikitifuliwa na kufunga raundi hio ya kumi na nane. Luanda sportiff watawakaribisha Butali katika uga wa Mumboha nao Sigalagala wakiwatembelea Vihiga Sportiff katika uga wa shule ya upili ya Kegoye. Lumakanda watatifua kivumbi dhidi ya Lugulu ndani ya uga wa Lumakanda nao Emuhaya wakitesa nyasi ana kwa ana na Rosterman ugani Ebunangwe.

Hatimaye Green Canopy watasafiri hadi Lunyofu grounds kuvaana na Marenga .

Kufikia sasa ligi hio inaongozwa na Compel wakifwatwa na Vihiga huku Bungoma Allstars wakifunga tatu bora.

Baada ya raundi hio ya kumi na nane mshindi wa kipute hicho atavaana na mshindi wa Zone B Kutafuta timu ambayo itajiunga na ligi ya daraja la pili almaarufu National Super League.

Hata hivyo waandalizi wa mitanange hio wamelalamikia ukosefu wa rasilimali za kuandaa mechi hizo ambazo ni pamoja na mipira ya kutosha, marupurupu ya waamuzi, jezi za wanasoka na mbinu za usafiri.

Kulingana na Wilbright Juma Busolo mwenyekiti wa Kanzu FC kamati shikilizi ya FKF imefeli kuwezesha matukio ya kipute hicho sawasawa na tume ya FKF iliyovunjwa na Waziri wa michezo Bi. Amina Mohammed.

Hivyo basi waandalizi hao wameiomba serikali pamoja na tume husika kuhakikisha wanawapiga jeki vijana wapenzi wa soka

admin

admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *