Madarasa 28 kujemgwa kwa mwezi mmoja Nyandarua Kaskazini

Awamu ya pili ya ujenzi wa madarasa ya CBC katika Kaunti ndogo ya Nyandarua Kaskazini, imeanza.

Akiwatangazia wajenzi na wanakandarasi wa ujenzi kufunguliwa kwa awamu hiyo, Mkuu wa Elimu katika eneo hilo Justus Musyoka, alisema kuwa jumla ya madarasa 28 yanatarajiwa kujengwa, katika shule 14.

Ujenzi huo, unatarajiwa kukamilika kwa muda wa mwezi mmoja ili kuwapa wanafunzi wa gredi la sita nafasi katika shule za upili kufikia January mwaka ujao. “Wanakandarasi watakaoteuliwa kuyajenga madarasa haya, watajulishwa wiki ijayo ili waanze kazi ya ujenzi haraka iwezekanavyo,” alihoji Musyoka.

Akijuta kuwa ongezeko la bei ya bidhaa haukuangaziwa katika mugawo wa pesa za kandarasi hizo, Musyoka alidai kuwa tayari Baraza la Mawaziri lilikuwa limeidhinisha malipo hayo.

“Wengi wa wajenzi hawa wametuomba tuongeze pesa lakini jambo hilo haliwezeka kwa sasa, maana Baraza la Mawaziri lilikuwa tayari limeidhinisha mgao wa awali, wa Sh788, 220, kwa kila darasa, pasi na kuzingatia uongezeko wa gharama ya maisha,” alisema Musyoka.

Jumla ya shule 14 zikiwemo shule ya wasichana ya Ndaragwa, ya wavulana Leshau, na za Miseyo Irigithathi na Githungucu, zitanufaika katika ujenzi wa madarasa mawili, kwa kila shule, huku wakuu wa shule hizo wakitakiwa kuwasaidia wajenzi hao, ili kukamilisha miradi kwa wakati.

“Tunawahimiza wakuu wa shule kuwapa mafundi hawa usaidizi wa hali na mali ili kuwawezesha kukamilisha madarasa kwa wakati. Awamu ya Kwanza ilikumbwa na changamoto si haba, ikiwemo kucheleweshwa kwa miradi na wengine hata kususia kazi kwa madai ya malipo duni,” alisema Naibu wa Kamishna wa eneo hilo Walter Ngaira.

Tayari madarasa yameshakamilishwa katika awamu ya kwanza, huku migao mingine ya pesa za miradi kwa mashule kupitia Wizara ya Elimu na mgao wa miradi kwa kila mwanafunzi inaendelea, na hivyo basi inatarajiwa kuwa bodi za shule zitatia bidii katika ujenzi ili kumudu kiwango mara dufu cha wanafunzi watakaojiunga na shule hizo mwaka ujao.

admin

admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *