Wakaazi waamkia kuupata mti mtakatifu umeanguka

Wakaazi wa Pokot Magharibi wamepigwa na butwaa baada ya kuamka asubuhi na kuupata mti wa kihistoria unaoaminika kuwepo kwa zaidi ya milenia moja ukiwa umeanguka kufuatia mvua kubwa iliyokunya Jumatatu usiku.

Wazee, vijana kwa watoto walifunga safari kuelekea maeneo ya Bendera kando ya barabara kuu ya kutoka Kapenguria kuelekea Lodwar ili kuutazama bila kuuguza mti huo unaojulikana na wenyeji kwa jina la kijumla kama simotwo (fig tree).

Kulingana na baadhi ya wakaazi wa eneo hilo la Bendera, huenda mti huo ulianguka baada ya saa tatu usiku maana walipopita sehemu hiyo jana usiku ulikuwa bado umesimama.

Walisema ni miujiza kwao maana mti huo haukuelekea sehemu kuliko na nyaya za nguvu za umeme wala kwenye barabara hiyo kuu maana ungesababisha madhara makubwa.

“Tulikuwa tumelala na hatukuskia mti huu ukianguka. Unavyouona ulianguka kwa utulivu bila kuelekea kwenye lami wala laini kuu ya stima ambazo ziko mita chache kutoka kwenye shina la mti huo,” mkaazi mmoja alisema.

Aidha wakaazi hao walisema kuwa iwapo mti huo ungeanguka mchana, nyuki wanaoishi katika mti huo wangevuruga shughuli za wakaazi.

Mti huo wa kiasili unaosemekana kusheheni itikadi za kitamaduni ulikuwa umejitwiga pembeni mwa barabara hiyo kuu na huenda iwapo barabara hiyo ingepanuliwa zaidi ungelazimu ung’olewe jambo ambalo wazee ya jamii ya Wapokot hawangeruhusu.

Kulingana na mtaalamu ya utamaduni wa jamii ya Wapokot Mzee William Lopetakou, mti huo kwa jina la kiasili simotwo ni aina ya mnagei (ficus natalensis) kutokana na maumbile yake ya kupindapinda tofauti na aina nyingine za asili hiyo.

Mzee Lopetakou alifafanua kuwa mti huo ndilo chimbuko la Lokesheni ambayo iliitwa Mnagei ambapo kwa sasa ni taarafa katika kaunti ndogo ya Pokot Magharibi.

“Wakati fulani wazee walilazimika kupeleka malalamishi yao kwa serikali baada ya kusemekana mti huo ungekatwa wakati wa kupitisha laini ya stima katika sehemu hiyo. Inaaminika kuwa wazee na wamorani walikuwa wakiaandaa mikutano yao hapo wakati wa kutoa Baraka kwa wakaazi kabla ya ukoloni,” alieleza Mzee Lopetakou.

Hali kadhalika jamii ya Wapokot kwa ujumla inauenzi mti huo aina ya simotwo na katika sherehe za harusi wazazi huwa wanawabariki watoto wao kwa kurejelea mti huo.

Katika sherehe za harusi mara nyingi maharusi huambiwa: “Iliku sokon kilenye simotwo, isach kilenye simotwo, itopo le simotwo” inayomaanisha wafanikiwe kuwa matajiri kama mti wa simotwo, wanawiri kama mti wa simotwo na kupata watoto wengi na kupanua familia yao kama mti huo.

Akizungumza na KNA, Mzee Lopetakou aliwashauri wakaazi kutokuwa na wasiwasi wowote huku akiwatahadharisha dhidi ya kuanza kutoa maelezo yanayopotosha kuhusu kuanguka kwa mti huo.

Wakaazi wamesema kuanguka kwa mti huo umefanya sehemu hiyo kupoteza ulimbwende wake maana mti huo umekuwa ni kivutia kwa na wapita njia katika barabara hiyo kuu ya kuelekea kaunti ya Turkana.

Mti huo kutokana na ukubwa wake unawasetiri ndege, wanyama pamoja na nyuki ambao wameunda makaazi yao na wakati tulipofika katika sehemu hiyo, walikuwa wanaendelea na shughuli zao za kutengeneza asali.

admin

admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *