Wajane kunufaika na hazina ya Thamini Mjane

Wajane katika kaunti ya Elgeyo Marakwet watanufaika na mikopo ambayo haina riba kutoka hazina ya Thamini Mjane kutoka kwa serikali kuu.

Akizungumza alipozindua hazina hiyo mjini Iten katibu mwandamizi katika wizara ya wafanyi kazi wa umma Jebii Kilimo aliwataka wajane hasa wa kivita kutoka kanda ya bonde la Kerio kujitokeza kuchukua mikopo kutoka kwa hazina hiyo ili kujiimarisha kimaisha.

Bi. Kilimo alisema hazina hiyo iliyoanzishwa na rais Uhuru Kenyatta mwaka jana tayari imetoa takriban shillingi Milioni 10 kwa vikundi mbali mbali vya wajane kote nchini.

Katibu huyo mwandamizi hata hivyo aliiomba serikali kufungua masoko mbali mbali ambayo yamefungwa katika eneo la bonde la Kerio kutokana na ukosefu wa usalama ili kuwawezesha akina mama watakaochukua mikopo hiyo kufanya biashara.

“Tunaisihi serikali kurejesha usalama katika eneo la bonde la Kerio ili masoko yaweze kufunguliwa na akina mama wetu waweze kushiriki katika shughuli za kibiashara,” alisema bi. Kilimo.

Bi. Kilimo alisema ana imani kuwa akina mama hao wataweza kufanya biashara na kulipa mikopo hiyo akisema licha ya changamoto za ukosefu wa usalama, akina mama kutoka eneo la bonde la Kerio wamekuwa wakichukua mikopo kutoka kwa hazina zingine za serikali na kulipa.

Katibu huyo mwandamizi alisema idara yake imehakikisha kuwa wajane katika kaunti za za Elgeyo Marakwet, Baringo na Pokot magharibi wamehamasishwa kuhusu hazina hiyo akisema wote wanapitia hali sawa baada ya waume wao kuuawa kutokana na wizi wa mifugo.

“Hii ni njia moja sio tu ya kuwapa uwezo wa kiuchumi akina mama hawa bali pia kuleta amani katika jamii hizi kwani watashirikiana wanapofanya biashara,” alisema bi. Kilimo.

Bi. Kilimo aliyekutana na akina mama hao katika ukumbi wa chuo cha mafunzo ya matibabu mjini Iten alisema alifurahi kuona kuwa wengi wao tayari wamejiunga katika vikundi kwani wametimiza mojawapo ya masharti ya kupata mikopo kutoka kwa hazina hiyo.

Aliwataka kuzuru afisi za jinsia katika kaunti zote ndogo ili kupata fomu za kupata mkopo huo na kuhakikisha kwa wanalipa ili waendelee kunufaika na fedha hizo.

Aliirai serikali ya kaunti ya Elgeyo Marakwet kuwawezesha akina mama hao kuzuru maeneo tofauti tofauti nchini kuona vile wajane wengine wamenufaika na hazina hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka jana.

admin

admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *