Mimba za mapema Igwamiti

Mimba za mapema ni swala linaloendelea kuathiri kwa kiwango kikubwa vijana hasa walio na miaka kuanzia 13 hadi 19 katika wadi ya Igwamiti kaunti ya Laikipia.

Wakaazi wa eneo hili wanadokeza sababu mbali mbali zinazochangia kuongezeka kwa janga hili.

Albert Omar anasema kuwa sababu kuu ambayo imechangia tatizo hili ni umaskini uliokita mizizi katika jamii kwani ukosefu wa mahitaji ya kimsingi hupelekea vijana hawa kujihusisha kimapenzi aghalau wafaidike kutoka kwa wapenzi hao.

“Pia shinikizo kutoka mitandao ya kijamii, kwani vijana hupenda kutazama video mbali mbali za ngono hivyo basi, pia wao hutaka kushiriki. Vile vile wazazi wengi hawajawajibika ipasavyo kuwapa watoto wao mafunzo namna ya kujitunza,” asema Omar.

Kulingana na Edinah Muthoni, tatizo hili linachangiwa na yafuatayo; vijana kujihusisha na matumizi ya madawa ya kulevya ambayo wakitumia huwa hawajielewi na kuwapelekea kujihusisha na mapenzi kiholela holela.

“Shinikizo la rika pale ambapo hutaka kufanya yale wenzao wanayoyafanya ili waweze jihisi kuwa wamo katika kundi hilo,wengi wa vijana hujihusisha na kufanya mapenzi wakiwa wadogo jambo linalopelekea wengi kupachikwa mimba bila kutarajia,” asema Muthoni.

Kulingana na Alice Ndung’u anawalaumu wazazi kwa kukosa kuwaadhibu watoto wanapopotoka kitabia jambo linalofanya kujihisi kuwa wao ndio wanatawala na hamna lolote wanaloweza ambiwa.

Pia aliongezea kuwa mizozo ya mara kwa mara miongoni mwa wazazi, imechangia watoto kupoteza mwelekeo kwani muda mwingi wazazi hawa huwa wanamakinika sana katika kusuluhisha migogoro yao na kukosa katika kuwajibika kulea watoto kwa njia inayofaa.

Anaongezea kwa kusema watoto wengi hasa wanaolelewa na mzazi mmoja huwa ni vigumu kudhibitika kwa kuwa huwadharau wazazi wao na kukosa kuwaskiza.

Kulingana na utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya nchini,takwimu zinaashiriwa kuwa takriban vijana 45,724 wameathirika na tatizo hili.

admin

admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *