Kikosi cha soka cha Bungoma Superstars kimepata pigo kubwa baada ya kupoteza mtanange wao dhidi ya Soy United wikendi hii na kusalia na matumaini finyu ya kufanya vyema kwenye mashindano ya shirikisho la soka nchini daraja la kwanza, kanda ya magharibi.
Hadi kufikia sasa, wana-Superstars wanashikilia nafasi ya kumi na tano ikiwa ni nafasi ya pili kutoka nyuma na kujiweka katika hatari ya kuangukiwa na shoka la kushushwa daraja.
Kikosi hicho kilifanya vyema msimu uliopita kwenye mashindano hayo na kumaliza katika nafasi kumi bora lakini msimu huu maji yamezidi unga. Wanadinga hao wamesakata mechi ishirini na mbili na kuvuna ushindi mara tatu pekee.
Wametoka sare mara tano na kubamizwa mara kumi na nne ya hivi punde ikiwa ni dhidi ya Soy United Jumamosi hii uga wa uwanja ndege mjini Bungoma.
Kwa mujibu wa wachanganuzi wa soka, itawawia vigumu Superstars kukwepa shoka la kushushwa daraja huku zikiwa zimesazwa mechi chache mno ligi hio kufikia kilele.
Miamba hao wa Bungoma hawajavuna ushindi katika mechi zao tisa za hivi punde wakiwa wamebamizwa mara nane na kutoa sare tasa dhidi ya Nyota FC mnamo tarehe kumi na tano mwezi wa sita.
Tarehe sita mwezi huu wa saba, kikosi hicho kitasafiri ugenini kuwavaa wana G. D. C FC ambao walivuna ushindi wa bao moja kapa dhidi ya Mayenje Santos wikendi iliyopita.
Kitakuwa kibarua kigumu kwa kikosi cha Superstars kuvuna ushindi dhidi ya kikosi cha G. D. C FC ambacho kimekuwa na matokeo mazuri, wakiwa wamevuna ushindi mara nne, kutoka sare mara mbili na kupoteza mara tatu pekee katika mechi tisa za hivi punde.
Vikosi hivi viwili vilipovaana na kutesa nyasi mara ya mwisho, wanasoka wa Superstars walivuna ushindi wa bao mbili kwa moja dhidi ya G. D. C ikiwa ni rekodi ya kipekee itakayowapa Superstars nguvu ya kuwavaa washindani wao, Jumatano hii.
Kwa mujibu wa msimamo wa jedwali la mashindano hayo, vikosi vya Bondo United, Sunderland, Bungoma Superstars na Elim FC vinashikilia nafasi nne za mwisho huku Bondo na Sunderland wakiwa na alama kumi na tano, Superstars wakiwa na alama kumi na nne nao waburura mkia Elim FC wakiwa hawajavuna alama hata moja.
Kati ya vikosi hivi vinne, vikosi vitatu vitashushwa daraja mwishoni mwa msimu na Bungoma Superstars wamo kwenye hatari ya kupigwa na shoka hilo.