Utata wa chama cha Ford Kenya Bungoma

Chama cha Ford Kenya kinachoongozwa na Seneta wa Bungoma Moses Masika Wetang’ula kipo katika hatari ya kupoteza umaarufu wake eneo la Bungoma huku baadhi ya wanasiasa tajika eneo hilo wakiwa tayari wamejitenga na chama hicho.

Hadi kufikia sasa, uhasama baina ya aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho mbunge wa Tongaren Daktari Eseli Simiyu na aliyekuwa kinara wake Moses Wetang’ula umezidi kukita mizizi huku wawili hao wakikashifiana hadharani katika mikutano ya kisiasa.

Kwa mujibu wa Eseli, Seneta Wetang’ula amekuwa akitumia umaarufu wa Ford Kenya eneo hilo kuwateua viongozi wa laiki yake na kukandamiza demokrasia ya watu wa Bungoma.

Mapema mwaka jana, chama cha Ford Kenya kilishuhudia kizaazaa huku gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati, mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi pamoja na mbunge wa Tongaren Eseli Simiyu wakielekea mahakamani kujaribu kubadili usimamizi wa chama hicho ambapo walilalamikia uongozi duni wa Wetang’ula.

Hata hivyo, Wetang’ula alipata ushindi katika kesi hiyo baada ya Desma Nungo mwenyekiti wa jopo la kuamua kesi hiyo kusema kwamba walalamishi hawakuzingatia kipengee cha 40 cha vyama vya kisiasa nchini katika malalamishi yao.

Ushindi wa Wetang’ula ulipasua chemichemi ya mpasuko chamani ambapo alimpoteza mbunge wa Kanduyi na gavana wake ambao wote walikiasi chama hicho na kujiunga na chama cha DAP-K cha Eugene Wamalwa.

Mpaka kufikia sasa, chama cha DAP-K kinaonekana kuwa tishio la Ford Kenya katika uchaguzi wa Agosti tisa, huku wagombea wakuu na wapinzani wa Ford Kenya katika uchaguzi huo wakiwa wafwasi wa chama hicho.

Katika kinyang’anyiro cha ugavana, farasi wawili Kenneth Makelo Lusaka wa Ford Kenya atavaana na Wycliffe Wangamati wa DAP-K ambao walivaana katika uchaguzi wa 2017.

Wangamati alimbwaga Lusaka katika uchaguzi wa mwaka 2017 alipojizolea kura 172,441 huku mpinzani wake akizoa takriban kura 150,465.

Hata hivyo, upinzani wa wawili hawa umekita mizizi huku kila mmoja wao akijisatiti kusanifisha chama chake.

Iwapo Lusaka atapoteza katika uchaguzi huo, chama cha Ford Kenya kitapata pigo kubwa kwani Wangamati ataingia ikulu ya Bungoma kwa tiketi ya DAP-K na kuandikisha historia kwani magavana wote wawili tangua kugatuliwa uongozi wameongoza Bungoma kwa tiketi ya Ford Kenya.

Kampeni za Lusaka na Wangamati zilizoa zogo mwaka wa 2017 huku wawili hao wakitozwa faini ya shilingi milioni moja kila mmoja baada ya kuripotiwa maafa katika kampeni zao jambo ambalo limeonekana kulegeza makali ya kampeni zao mwaka huu.

Katika ushindi wao wote, Lusaka na Wangamati walipendekezwa na Moses Wetang’ula kwa tiketi ya Ford Kenya jambo ambalo sasa linazidi kuwa kinaya katika uchaguzi huu.

Kando na kiti cha ugavana, baadhi ya Wabunge hodari wa Bungoma huenda wakashinda bila ya tiketi ya Ford Kenya mmoja wao akiwa mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi ambaye amekuwa mbunge wa Kanduyi kwa tiketi ya Ford Kenya kwa mihula mitatu ikiwa ni mwaka 1997, 2013 na mwaka wa 2017.

Iwapo Wamunyinyi atakitetea kiti chake kwa tiketi ya DAP-K, litakuwa pigo lingine kwa Wetang’ula kwani eneo bunge hilo ndilo eneo bunge kubwa mno Bungoma na lenye usemi mkubwa sana katika siasa za jimbo hilo.

Zaidi ya wabunge, mtetezi wa kiti cha uwakilishi wa wanawake Bungoma Catherine Wambilianga kwa tiketi ya Ford Kenya ana upinzani mkubwa huku wapinzani wake wakuu Reginalda Wanyonyi wa DAP-K na Nancy Kibaba wa UDA wakiwa wamejitoa jino kwa ukucha kumpokonya tonge lake mdomoni.

Kwingineko wawakilishi wadi waliokuwa ndani ya Ford Kenya sasa wanatetea viti vyao wakitumia vyama vingine.

admin

admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *