Vijana waonywa kutumiwa na wanasiasa kuleta vurugu msimu huu wa uchaguzi

Vijana katika kaunti ya Kitui wameonywa dhidi ya kutumiwa na wanasiasa kuvuraga amani.

Akizungumza kwa hafla iliyowaleta vijana na vikundi tofauti vya akina mama pamoja katika kaunti ya Kitui ya kati, naibu kaunti kamisheni Kitui ya kati Bi Dorcus Rono amewauliza vijana kukataa kutumika na wanasiasa kuleta vurugu na kuvuruga amani wakati huu wa uchaguzi.

Rono amewaomba hao kuwa mabalozi wa amani kama njia ya kuelemisha wananchi umuhimu wa kufanya uchaguzi wa amani.

“Ni jukumu la kila mmoja wetu kuhubiri amani na kuhakikisha uchaguzi huu wa Agosti ni wa Amani,” asema Rono.

Rono aliongeza kwamba uchaguzi ni shughuli ambayo hufanyika kila baada ya miaka mitano na basi haifai kuwa chanzo ya kukosana na jirani yako.

“Siasa huja na kupita, miaka tano iliyopita zilikuwa, miaka tano baadaye tunapiga kura, hivyo hili si jambo ambalo linaweza kufanya amani tumeishuhudia katika nchi yetu kuvurugwa. Vijana ninawaonya msije kamwe mkatumiwa na mwanasiasa yeyote kuzua vita,” akasisitiza.

Rono amesema kwamba kila mwanasiasa anahitajika kutia sahihi Mkataba wa Amani almaarufu Peace Charter.

Katika barua iliyoandikwa na Askofu mkuu wa Kanisa la Katoliki Kitui Josephe Mwongela wiki jana, amewahimiza wananchi kudumisha amani hasa wakati huu wa uchaguzi mkuu.

Barua hiyo ilieleza kwamba vita vya kisiasa vimeacha wengi walemavu, wengine wameadhirika kisaikolojia na wengine wamepoteza makao.

“Naomba washirika na wananchi wote wawe wapenda amani na kuwa mabalozi katika kueneza amani nchi yetu hususan wakati huu wa uchaguzi mkuu,” asema Mwongela.

Mashirika yasiyo ya kiserikali kama UN Women, Caritas, Red Cross, National Council of Churches of Kenya (NCCK), Federation of Women Lawyers yamehapa kushiriki na serikali katika kuhakikisha uchaguzi wa amani utashuhudiwa nchini.

admin

admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *