Wadau washirikiana kukabili athari za ukame Kilifi

Wadau mbalimbali katika kaunti ya Kilifi wakiongozwa na Mamlaka ya Kudhibiti Ukame nchini (NDMA) wameshirikiana katika juhudi za kukabiliana na athari za ukame zinazowakumba wakaazi wa kaunti hio ikiwemo ukosefu wa chakula.

Kongamano lililofanyika mjini Kilifi lilileta pamoja mashirika yote ya misaada, vitengo vya serikali kuu na vya serikali ya kaunti ili kujadili jinsi watakavyofanya kazi pamoja ili kuhakikisha usawa wa ugavi wa misaada kwa waathiriwa wote wa ukame.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Mratibu wa Mamlaka ya Kudhibiti Ukame Kaunti ya Kilifi Bwana Adam Ndamungu, zaidi ya wakaazi 72,000 kutoka sehemu kame Kilifi wanahitaji msaada wa dharura kutokana na baa la njaa na kukosa mahitaji ya kimsingi.

Katika mahojiano na wanahabari baada ya kukamilika kwa ripoti ya ushirikishi, siku chache baada ya kongamano, Bwana Ndamungu alisema mamlaka hio inasaidiana na wahusika wote kutoa huduma za kimsingi ili kuwanasua wakaazi kutokana na janga la ukame.

“NDMA tuna mipangilio ya kutoa udongo kwenye mabwawa, mojawapo ni Shomela ambalo lilikua limejaa udongo, kuna lingine Kayafungo tunataka tufanye na pia tuweze kuhakikisha kwamba tunashirikiana na wadau wengine,” alisema.

Katika ripoti yake, Bw. Ndamungu alieleza kuwa shirika la Plan International limesaidia shule zaidi ya 20 katika mpango wa Lishe Shuleni na kusaidia watu zaidi ya 3,000 katika mpango wa chakula kutoka sehemu mbali mbali kama ikiwemo Ganze, Bamba na Magarini.

Hata hivyo, kwenye mikakati ya kukabiliana na athari za ukame, washirika wengi ikiwemo Shirika la Chakula Duniani (WFP), Give Direct na World Vision walionekana kutilia maanani zaidi misaada ya kugawanya pesa taslimu kwa njia ya simu ili kuwezesha waathiriwa kununua chakula na kukidhi mahitaji mengine kama vile karo.

Huduma ya kusaidia watu kwa njia ya kupeana pesa iliyoanzishwa na serikali kuu katika mpango wa Inua Jamii, sasa imeshika kasi huku mashirika mengi yakigeukia mpango huo baada ya kugundua ubora wake.

Huku wadau wakikumbatia mpango huo, Bw. Ndamungu alieleza kuwa kuna uhitaji wa ushirikiano kati ya wadau ili kuzuia familia chache kupata misaada mara nyingi kuliko wengine.

“Juzi tulikuwa na kikao na washikadau wote ambao wanashugulika kusimamia mambo ya ukame. Tukakubaliana kwamba kwa sababu walioathirika katika kaunti ni takribani 72,000, ule mchakato wa kugawanya pesa tushirikiane pamoja wadau wote ili kila mtu aweze kusaidika na huu mradi,” alisema Bw. Ndamungu.

Shirika la Chakula Duniani (WFP) tayari limelenga familia 6,057 zilizoathirika na ukame ili waweze kusaidika na mpango kupewa kiwango cha Sh 6,500 kila mwezi kwa kila familia kwa muda wa miezi sita.

“Tulianza kukusanya majina tarehe 27 Julai, tukafanya usajili na kufikia wiki hii, kumefanikiwa kusajili watu 6,037, tumebakisha familia 20 tumalize. Kuna utafiti wa kimsingi unaendelea na kufikia tarehe 15 tutaanza kupeana pesa kwa walengwa,” alisema Bw. Jairus Mutisya, Afisa wa Ugavi na Usafirishaji wa vitu shirika la chakula duniani.

Kutokana na idadi kubwa ya watu wanaohitaji msaada, kiongozi wa Shirika la Chakula duniani Kaunti ya Mombasa Clara Silver alisema liko tayari kushirikiana na serikali zote pamoja na mashirika mengine kwa minajili ya kufikia watu wengi iwezekanavyo.

“Hali hii imechangiwa na mambo mengi kama kufeli kwa mvua zaidi ya misimu mine, vita vya Ukraine na hata mabadiliko ya anga duniani kote. Kwa kweli tunatazamia kutafuta njia endelevu ambapo tunaweza kufanya kazi pamoja kutafuta suluhu na kusaidia familia hizo za Kilifi kwa njia bora aidi,” alidokeza Silver.

Aidha alikiri kwamba pesa hizo ni chache mno ikizingatiwa gharama ya juu ya maisha inayotokana na mfumuko wa bei ya bidhaa muhimu. Hata hivyo alisema mpango wa kuleta pamoja wadau wote itasaidia kupata suluhu la kudumu.

admin

admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *