Wanasiasa waonywa kutotumia pombe kuwarai wafuasi wao kuwapigia kura

Naibu kamishna wa gatuzi dogo la Molo, Josephat Mutisya amewaonya vikali wanasiasa dhidi ya kuwahonga wafuasi wao kwa kutumia pombe.

Mutisya alisema kuwa njia hii ya kuwafurahisha wafuasi wao wakati wa kampeini ni potovu kutokana na madhara yanayosababishwa na unywaji pombe haramu na hivyo basi kuwataka kufanya kampeini zao kwa utulivu kwa kutumia mbinu sawa.

Aliendelea kusema kuwa inasikitisha kuona kuwa wale wanaoibugia pombe hii hunywa kupita kiasi na kusababisha vurugu, kushindwa kufanya kazi yoyote ile itakayowezesha kulisha familia zao na wengine hata kuitegemea mara kwa mara wakitorokea majukumu muhimu ya kifamilia.

Wanasiasa wanaoendeleza tabia hii wanawapotosha vijana na vile vile wanaikosea jamii pamoja na afisi husika za serikali zinazopiga vita unywaji pombe haramu kwa kuzima juhudi zao.

Hata hivyo, alisema kuwa wale watakaokiuka agizo hili bila shaka watachukuliwa hatua ya kisheria akiongezea kuwa ni muhimu kampeini kuendeshwa kwa amani na kuwapa vijana mawaidha yatakayo wajenga kimaisha.

Mutisya alikuwa akizungumza wakati wa hafla ya 59 ya siku ya Madaraka iliyoandaliwa katika uwanja wa Molo.

Baadhi waliokuwepo ni pamoja na mwakilishi wadi ya Molo, Michael Karanja, mbunge wa eneo hili, Kuria Kimani pamoja na viongozi wengine wanaowania nyadhfa mbalimbali. Walitoa ujumbe wa amani wakati na baada ya uchaguzi.

Wakiwahutubia wananchi, wanasiasa hao waliwasihi wakaazi kutogawanyika katika misingi ya kikabila bali wapendane na majirani zao. Walihitajika kuwa kielelezo chema kwa kuwa mstari wa mbele kuwasuta wanasiasa walio na nia ya kuvuruga amani iliopo.

admin

admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *