Watoto 159 kuishi bila virusi vya ukimwi

Watoto 159 kutoka kaunti ya Elgeyo Marakwet ambao walizaliwa na wazazi wanaoishi na virusi vya ukimwi wataishi bila virusi baada ya kupitia mpango mahsusi wa matibabu unaofadhiliwa na shirika la Ampath.

Kulingana na naibu mkuu wa shirika hilo Dkt. Jeremiah Laktabai matibabu hayo huanza pindi tu mama anaposhika mimba na kuendelea hadi pale mtoto anapofikisha miezi kumi na nane na kwa hivyo ni muhimu kwa akina mama wajawazito kuhudhuria kiliniki.

Alisema kaunti hiyo imekuwa mstari wa mbele katika mpango huo akielezea hii ni mara ya tatu kwa watoto zaidi ya mia kupata matibabu hayo.

Mkurugenzi wa afya katika kaunti hiyo Dkt. Patrick Kosgey alisema unyanyapaa bado ni changamoto katika vita dhidi ya ukimwi jambo ambalo huwafanya wengi kuficha hali yao au hata kutopimwa.

Dkt. Kosgey aliwataka wakazi kujua hali yao akisema hili litasaidia kuwakinga wengine na pia kuhakikisha watoto wanaishi bila virusi.

Bi. Lucy Ghati ambaye ni mkurugenzi katika baraza la kitaifa la kudhibiti ukimwi (NACC) aliwarai wakazi kuwapa moyo akina mama ambao wanajitokeza na kutangaza hali yao akisema hili litawapa nguvu wengine walio na virusi kujitokeza.

Alisema alifurahia kuona waume kadhaa ambao waliandamana na wake zao na watoto katika hafla hiyo akisema ni muhimu kwa familia kusimama pamoja ili kukabiliana na ukimwi.

Pia aliwataka akina mama kuhakikisha kuwa wanajifungua katika vituo vya afya akisema kando na kuwa serikali inatoa huduma hii bure, watoto wao watapata matibabu yanayofaa.

admin

admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *