Watu wawili wapoteza maisha huku wengine wakijeruhiwa

Watu wawili waliaga dunia hapo jana huku wengine wawili wakiendelea kuuguza majeraha katika hospitali kuu ya Iten baada ya mashambuliano kati ya maofisa wa misitu na wakazi katika kijiji cha Musekekwa kaunti ndogo ya Keiyo Kaskazini.

Inasemekana kuwa mtu mmoja alifariki papo hapo huku mwingine akifariki pindi tu alipofikishwa hospitalini baada ya kupigwa risasi na maafisa wanaolinda msitu wa Musekekwa.

Mkuu wa Polisi katika eneo hilo Tom Makori alisema mnamo jumatatu maafisa wanaosimamia msitu huo wa serikali waliwazuia kondoo 22 waliopatikana wakiwa malishoni katika msitu huo na kuharibu miche iliyokuwa imepandwa.

“Hakukuwa na mtu aliyekuwa anawachunga kondoo hao na hivyo ikabidi wazuiliwe hadi pale mwenyewe angeljjitokeza,” alisema Makori.

Hata hivyo mnyama pori ambaye bado hajulikani aliwavamia usiku na kuwaua kondoo 20 jambo ambalo liliwatia hamaki wakazi ambao waliandamana na kuvamia kituo hicho cha misitu.

Kulingana na Makori, wakazi hao waliharibu baadhi ya vifaa katika kituo hicho akisema maafisa wa polisi wameanzisha uchunguzi mara moja kutathmini wananchi walioumizwa na pia thamani ya vifaa vilivyoharibiwa.

Mkuu wa shirika la wanyama pori nchini katika kaunti ya Elgeyo Marakwet Zablon Omulako aliwashauri wakazi kutochukua sheria mikononi mwao akisema wangeripoti kisa hicho kwa afisi yake ili wafidiwe kwa vile kondoo hao waliuawa na mnyama pori.

“Ikiwa maofisa na wakazi wangeshirikiana jambo kama hili halingetokea kwani serikali huwa inawafidia watu ambao wanapoteza mifugo wao baada ya kuvamiwa na wanyama pori,” alisema Omulako.

Naibu wa Mkuu wa Kaunti Julius Maiyo alisema serikali itachunguza kisa hicho na kuchukua hatua kwa yeyote atakayepatikana na hatia na akawataka wakazi kujitokeza kutoa ushahidi bila kuogopa.

Alisema maofisa wote wa serikali wameajiriwa kuwahudumia wananchi na wala si kuwadhulumu.

Wananchi wameitaka serikali kulishughulikia swala hilo kwa dharura ili waliopoteza maisha yao na waliopata majeraha kupata haki.

admin

admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *