Yassin Sije aizamisha meli ya Nyota FC 

Wakali wa kandanda kutoka jimbo la Bungoma Nyota FC wamepata pigo ugenini baada ya kupoteza mechi dhidi ya Mayenje Santos mnamo Jumatano.

Kikosi hicho chake mkufunzi Ibrahim Shikanda kilipaisha matumaini yake mnamo Jumamosi baada ya kuandikisha ushindi dhidi ya Kona Rangers FC ila kipigo cha jumatano hii kilididimiza matumaini hayo ya kuingia katika nne bora za jedwali kwani mabingwa hao wamesalia na mchuano mmoja tu msimu huu dhidi ya Transfoc FC.

Mayenje Santos walifikia matarajio yao ya kuhakikisha wanafungua mwanya wa alama nne baina yao na Kona Rangers wanaoshikilia nafasi ya pili na kujihakikishia ubingwa wa ligi hio wakiwa wamesalia na mechi moja mkobani.

Licha ya Nyota FC kuonyesha umilisi mzuri wa mpira kipusa bahati alikataa katakata kusimama kidete kwa washambulizi wa kikosi hicho wakiwemo Long’o Moses, Bramwel Bukono almaarufu bosi na Allan Sereka kwani nafasi zao za wazi ziliishia kwenye mikono ya mlindalango wa Mayenje Santos Phanuel huku zingine zikipaapaa juu ya mtambaapanya.

Kitumbua cha Nyota kililamba mchanga mnamo dakika ya kumi na tatu baada ya jaribio la Mayenje Santos kuwazolea penalti iliyosukwa kiufundi na mshambulizi wao matata Yassin Sije almaarufu Bishop moja kwa moja hadi katika wavu wa Blaze Omwata mlindalango wa Nyota.

Kipindi cha kwanza kilikamilika moja kwa yai kwa faida ya Mayenje Santos huku wanasoka wa Nyota FC wakilalamikia maamuzi ya mwaamuzi wa mechi hio. Dakika za kwanza za kipindi cha pili zilijaa mihemko ya aina yake huku timu zote mbili zikiwavizia walindamilango pinzani kwa mikeke motomoto ya kusaka bao.

Yassin Sije alitia moto kwenye donda la Nyota FC baada ya kusuka pasi nyengine na kumwacha mlindalango wa Nyota FC Blaze Omwata akipaa angani pasi na mafanikio huku Mayenje Santos wakipanda kidedeani mabao mawili kapa.

Bao la tatu lilifwata muda si kiduchu baada ya walinzi wa Nyota kufanya masihara huku mshambulizi wa Mayenje Santos Wafula akipiga pasi nyerezi hadi kwenye guu la kushoto la muuaji Zola aliyejipinda kama pia na kufumua tofali lililojaza Kamba na kuwaweka Mayenje kifua mbele mabao matatu kapa.

‘’Tumekubali kupoteza dhidi ya Mayenje kwa kuwa asiyekubali kushindwa si mshindani na tunatarajia matokeo bora katika mechi yetu ijayo tutakayowaalika Transfoc,’’ mfungaji wa bao la kufutia machozi kwa Nyota FC Allan Sereka alisema kwenye mahojiano na meza ya spoti ya KNA.

admin

admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *